Hivi karibuni, nchi ya Rwanda iliadhimisha miaka 15 tangu yalipotokea mauaji ya Kimbari yaliyosababisha vifo vya karibu watu milioni moja.
Nchini Tanzania, ubalozi wa Rwanda uliandaa sherehe fupi ili kukumbuka na mauaji hayo na kupanga mikakati ya kuzuia yasitokee tena.
Akihutubia katika sherehe hizo, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Zeno Mutimura, anasema,
"Tunapoadhimisha miaka 15 ya mauaji ya Watutsi wa Rwanda, tunapaswa pia kujitazama tuko wapi, tunatoka wapi na tunaelekea wapi kama Taifa. Katika hali kama hiyo tunapaswa kuwa na majibu kwa maswali magumu kama yafuatavyo,
Nini chanzo, mchakato na utekelezaji wa mawazo yaliyosababisha mauaji ya Rwanda?
Mauaji ya kimbari ni asili ya Rwanda au yanaweza kutokea sehemu yoyote duniani?
Tumefanya au tunafanya juhudi gani sisi kama serikali ili kufuta giza nene lililoifunika historia yetu?
Je, tumepata somo gani kutoka kwenye mauaji hayo kama Rwanda wenyewe na ulimwengu kwa ujumla?”
anasema Balozi Mutimura.
Akieleza chanzo, athari na mipango ya Wakoloni iliyosababisha mauaji ya Kimbari ya Rwanda, Balozi Mutimura anasema,
"Kwa karne kadhaa Wanyarwanda wamekuwa wakitumi lugha moja, utamaduni mmoja na mazingira mamoja kama watu wa Taifa moja. Lakini utawala wa kikoloni ulifanya mbinu za kujjenga makundi ya kikabila na kuchochea chuki za kikabila pale walipoanzisha vitambulisho vilivyoainisha asili ya watu kikabila.
Hakuna anayeweza kupuuzia athari zilizotokana na mauaji hayo . Moja kati ya kumbu kumbu za mauaji hayo katika nchi yetu kama ilivyo kwa nchini nyigine yalipotokea, ni dhana ya mauaji na tabia yake ya kujirudia.
Ndiyo maana hili neno 'Mauaji ya kujirudia' limewekwa limepandikizwa na watekelezaji wa mauaji ya Wanyarwanda na wafadhili wao wa nje. Ili kuendeleza chuki dhidi ya Watutsi, wauaji hao wanaeneza fikra potofu kwamba kulikuwa pia na mauaji ya Wahutu yaliyotekelezwa na chama RPF na serikali ya Rwanda". anasema Balozi Mutimura.
Akieleza athari za dhana ya kulipiza kisasi katika mauaji ya kimbari, Balozi Mutimura anasema,
"Wauaji hawa wanaendelea kuua waliosalimika kwenye mauaji hayo. Hii inafanyika kama mpango unaoendelea wa kuwamaliza Watutsi ndani na nje ya nchi. Wanaendelea kuwaua waliosalimia ili kupoteza ushahidi unaopelekwa kwenye mahakama za jadi (Gacaca) na ile ya Mauaji ya Rwanda (ICTR) iliyoko Arusha. Wauaji hao walijaribu hata kulipua Makumbusho ya mauaji hayo."
Jambo la pili ni kuungana na Wafadhili wa nje wa mauaji hayo. Hii inafanyika kwa njia nyingi ikiwemo ya kuwatuhumu maafisa wakubwa wa jeshi la Rwanda kuwa walihusika na mauaji hayo wakati wao ndiyo waliojitahidi kuzuia mauaji hayo.
Mfano mzuri ni kukamatwa kwa Rose Kabuye aliyekamatiwa Ujerumani na kupelekwa Ufaransa akihusishwa na kudungua ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana.
Wakati tunayashuhudia mambo haya, tuna matumaini kuwa huu utakuwa mwisho wa udhalimu wa kimataifa unaotekelezwa na majaji kama vile Louis Brougierre na wengineo wan chi za Magharibi.
Jambo la tatu ni vita vinavyoendelea mashariki ya Congo. Wapiganaji wa Interahamwe walioshindwa vita Rwanda sasa wamejikusanaya katika muungano wao wa FDRL na kuunda jeshi ambalo limeanzisha mapambanao huko mashariki ya Congo.
Kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiua Wa Congo wasio na hatia kwa lengo lile lile la mauaji ya Rwanda kwenye mipaka ya Rwanda.
Ieleweke kwamba mwezi February mwaka huu, Serikali za Rwanda na DRC zimeunda umoja wa kijeshi unaojulikana kama UMOJA WETU ambao sasa umeiharibu ngome ya FDRL iliyoko mashariki mwa DRC na kuwakamata baadhi ya wapiganaji na wengine wamekimbilia Rwanda. Walikuwa zaidi ya 1000.
Tunaamini kuwa umoja huu utakuwa endelevu na wenye mafanikio makubwa hasa kwa nchi za maziwa makuu. Tunaamini kuwa huu ni mkakati wa ndani utakaomaliza matatizo ya Afrika.” anasema Balozi Mutimura.
Akitoa tahadhari kwa nchi nyingine kuhusu mauaji hayo, Balozi Mutimura anasema,
"Kimsingi mauaji ya Rwanda yalitokea kwasababu ya utawala mbaya wa kikoloni yaliyo uliokuwa ukipinga uzalendo. Utawala wa Kayibanda na Habyarimana baada ya ukoloni uilirithi na baadaye kutekeleza siasa za kikoloni nchini Rwanda mpaka rwanda ilipoingia kwenye mauaji ya kutisha yaliyoishtua dunia.
Haya yanaweza kutokea popote duniani kuliko na uongozi wa aina hii.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikifanya jitihada mbali mbali kufuta giza lililofunika historia yetu. RPF ilikomesha mauaji ya kimbari na kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa mnamo tarehe 19 Julai 1994 uliokuwa umepotea katika siasa na uchumi na kijamii.”
Hata hivyo bado Rwanda ina changamoto mbele yake,
"Changamoto iliyopo ni kuimarisha hali hii ili kuponya matatizo yaliyokuwepo yasitokee tena. Leo hakuna ubishi tena kwamba Rwanda imepata mafanikio ya kichumi, siasa na kijamii katika malengo yake ya mwaka 2020."
kutokanana na matatizo tuliyoyarithi baada ya kukomesha mauaji ya kimbari, tumeanzisha juhudi za awali ili kusuluhisha matatizo hayo.
Ndiyo maana tumeanzisha mahakama za Gacaca zenye mfumo wa kitamaduni uliokuwepo kabla ya wakoloni. Tulifikia hatua hiyo wakati nchi ilipokuwa inawashikilia watuhumiwa wa mauaji hayo zaidi ya 120,000 katika magereza.
Tangu wakati huo, Mahakama za Gacaca zimeshaamua kesi milioni moja na nusu kabla ya kumaliza muda wake baadaye mwaka huu.
Mahakama za kawaida nazo zimeshaamua kesi 10,000 wakati Mahakama ya Kimataifa ya kesi za Rwanda (ICTR) imeshaamua kesi 35 tu baada ya kutumia zaidi ya bilioni za dola za Marekani.”
Balozi Mutimura antoa ushauri kwa nchi nyingine,
"Uongozi wowote unaoendesha siasa za kuwagawa watu, unaweza kuwafikisha wananchi wake kwenye machafuko kama haya yaliyoifika Rwanda mwaka 1994.
Kushindwa kumaliza rushwa miongoni mwa viongozi, pia inaweza kuwa sababu yakuifikisha nchi kwenye machafuko. Tunaamini kwamba yaliyotokea Rwanda kwa siala la kuendeleza uchumi na jamii na msimamo wa kisiasa baada ya mauaji ya mwaka 1994, yatakuwa somo kwa jumuiya ya kimataifa." anasema Balozi Mutimura