KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk Khalid
Mohamed amependekeza nafasi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
katika Muungano itazamwe upya na kuondoa kero za Muungano.
Dk Mohamed alisema hayo alipotoa maoni mbele ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana, kwa niaba ya Watumishi wa Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Huku akisisitiza kuwa maoni hayo si msimamo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bali ni maoni ya Watumishi wa ofisi
hiyo, alisema Katiba Mpya itazame upya nafasi hiyo ili iwe kama Hati za
Muungano zinavyosema.
“Wakati Rais Nyerere (Julius) na Rais Abeid Amani
Karume wanakubaliana kuunda Muungano, kuna mambo walikubaliana katika
hati hiyo ya Muungano, kwamba Rais Nyerere awe Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kuwa Makamu
wa Rais katika Serikali ya Muungano,’’ alisema DK Mohamed.
Dk Mohamed alifafanua kuwa Katiba ya sasa
haionyeshi wala kumpa nafasi yoyote Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika masuala ya Muungano, hivyo tumependekeza katika Katiba
ijayo nafasi yake itazamwe upya.
Mbali na hilo, Dk Mohamed alisema pia
wamependekeza mambo ya Muungano yatazamwe upya katika Katiba ijayo ili
kuondoa malalamiko yaliyopo baina ya pande mbili za Muungano.
Alisema kwa sasa mambo ya Muungano yapo 22, lakini
kiukweli ni zaidi ya hayo yaliyopo sasa kwa sababu utakuta jambo moja
lina mambo mawili au zaidi.
Alisema ili hilo lifanikiwe ni lazima pande zote
mbili za Muungano zikutane na kuainisha kwa uwazi ni jambo lipi
linalohusu Muungano na mipaka yake ijulikane ili kufanya Muungano uwe
imara.
“Kubainisha mambo ya Muungano na mipaka yake ni
jambo la muhimu wakati huu ambao tunataka kuandika Katiba yetu, kwa
kufanya hivyo tutaweza kupata mifumo ya kikatiba ambayo itasaidia
kutekeleza mambo ya Muungano,” alisema Dk Mohamed.
Alisisitiza kuwa ili kufanya Muungano kuwa imara
Katiba ijayo iweke vyombo vya kusimamia mambo ya Muungano ambavyo
vitakuwa na sura ya kimuungano.
“Sura ya Muungano itakuwepo pale ambapo viongozi na watumishi wa vyombo hivyo vya Muungano watakuwa wanatoka katika pande zote mbili za Muungano na kwa uwiano sawa,” alisema.
“Sura ya Muungano itakuwepo pale ambapo viongozi na watumishi wa vyombo hivyo vya Muungano watakuwa wanatoka katika pande zote mbili za Muungano na kwa uwiano sawa,” alisema.
No comments:
Post a Comment